Hatima ya nyota wanaokipiga katika klabu ya Yanga Yannick Bangala na Djuma Shabani kuendelea kusalia Yanga itajulikana mwisho wa msimu huu wakala wao amethibitisha hilo.
Nyota hao kutoka nchini DR Congo walijiunga Yanga mwaka jana na wameisaidia Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC msimu huu mpaka sasa huku timu hiyo ikiwa na uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa.
Faustino Mukandila,Wakala wa wachezaji hao amesema hatma yao itajulikana mwisho wa msimu huu kama wataendelea kubaki Yanga au wataondoka.
“Ni kweli nimepokea ofa kutoka timu nyingi zikihitaji huduma yao lakini niseme kuwa kila kitu kitawekwa wazi baada ya msimu huu kuisha” Alisema Faustino
Hata hivyo alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuondoka Yanga Mukandila alisema mchezaji yoyote duniani anahitaji maslahi mazuri kila siku na uwezekano wa kucheza hivyo lolote linaweza kutokea
“Unajua mpira ni biashara kama biashara nyingine, mchezaji hana timu,yeye timu yake ni maslahi mazuri zaidi na uwezekano wa kucheza hayo mengine ni ziada hivyo ukifika muda wa kuondoka wataondoka Ila kwa sasa ni wachezaji wa Yanga na wana mkataba na Yanga tusubiri baada ya msimu tutaona nini kitafuata na kuhusu kuondoka kwenye mpira lolote linaweza kutokea” Alisema
Taarifa tulizonazo ni kwamba nyota hao huenda wakaondoka klabuni hapo mwisho wa msimu huu na kutimkia uarabuni ambako wanatajwa kutakiwa.
