Wakati ligi nyingi duniani zikielekea ukingoni na tukielekea kwenye dirisha kubwa la usajili,timu zimeanza maandalizi ya kuimarisha vikosi vyao kwa kusajili majembe mapya.
Klabu ya Simba inatajwa kumalizana na mshambuliaji wa Klabu ya Zanaco ya Zambia Moses Phiri na huenda akatua nchini Tanzania mapema mwezi ujao kuja kukamilisha dili hilo
Taarifa kutoka nchini Zambia zinasema tayari Moses Phiri amewaaga wachezaji wenzie kuwa anataka kutafuta changamoto mpya huku wakala wake akisema hakuna ofa aliyopokea mpaka sasa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Moses Phiri ameandika
“Msimu wa 2021-2022 umekamilika asanteni sana mashabiki wa Zanaco fc na wote waliotuunga mkono kwa kweli japo lengo halikukamilika hatukuwa na msimu mzuri..tunaendelea na tusubiri Alichotuandalia Bwana kwa msimu ujao 😊😊 Asante kwa mara nyingine”
Tulipomtafuta CEO wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez kuweka wazi hizi taarifa za kumalizana na nyota huyo alisema kwasasa ana majukumu mengi hata hivyo kama Simba bado wanaangalia namna ya kumaliza msimu huu kwanza ndipo wataangalia nani na nani watamsajili kulingana na pendekezo la Kocha.
“Kwasasa nina mambo mengi lakini haitapendeza kusajili wachezaji wapya wakati wapo wengine wanaendelea kuipigania timu,kwanza tunahakikisha tunawaongezea mikataba wachezaji muhimu ambao mikataba yao inaisha Kisha tutaangalia hapo baadae tutafanya nini kwa kuzingatia mapendekezo ya Mwalimu” Alisema Barbara.
