Baada ya tetesi kusambaa zikimhusisha Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba Pablo Franco Martin kutakiwa na Klabu ya Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini na Horoya ya Guinea,wakala wa Kocha huyo Edgar Mitema ameweka wazi hatma ya Kocha huyo kuendelea kukinoa Kikosi hicho cha wekundu wa msimbazi msimu ujao.
Mitema ambaye ni raia wa Kenya amesema hatma ya Kocha huyo bado ipo mikononi mwa Viongozi wa Simba kwani bado Pablo Franco ana mkataba wa mwaka mmoja.
“… Pablo Franco bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Simba na kuhusu kuendelea itategemea na viongozi wa Simba watakavyoamua mwisho wa msimu kwani kulikuwa na malengo aliyopewa na tayari moja ya lengo la Klabu ilikuwa kuifikisha Simba robo fainali ya CAF Confederation Cup na tayari ameshafanikiwa.. Lakini malengo mengine ni kutetea ubingwa wa ligi kuu na Kombe la FA ambapo Yanga wameanza kudondosha alama huku kwenye FA Simba wako robo fainali” Alisema Edgar Mitema
Alipoulizwa kuhusu ofa za Orlando Pirates na Horoya alisema walipokea ofa hizo kabla ya droo ya hatua ya makundi ya CAF Confederation Cup.
Hata hivyo alikiri kuwa ofa za vilabu hivyo (Orlando Pirates na Horoya) ni kubwa hivyo wanasubiri mwisho wa msimu waone watafikia malengo kwa asilimia ngapi ya Klabu ya Simba huku akiwasikiliza zaidi viongozi wa Simba maamuzi yao.
