Licha ya kupewa onyo na Shirikisho la Soka Barani Afrika,Kocha msaidizi wa Klabu ya Orlando Pirates ya nchini Afrika Kusini Mandla Ncikazi amegoma kuiomba msamaha Klabu ya Simba ya nchini Tanzania kwa kauli alizozitoa.
Ncikazi amethibitisha kupokea barua ya onyo ya CAF na kukiri Makosa yake lakini amegoma kuomba radhi kwa matamshi yake ya kuchukuliwa kama wanyama na Klabu hiyo ya Nchini Tanzania walipokwenda kucheza mchezo wa robo fainali mzunguko wa kwanza.
“Nadhani CAF ilielewa kilichokuwa kwenye barua ya majibu yangu,Niliomba radhi kwa CAF labda matamshi yangu nilisema sehemu isiyo sahihi,Tungeweza kuwasilisha kwa njia tofauti..lakini waafrika lazima tubadili msimamo huu kwamba timu pinzani ikienda nchini Tanzania wanaweka uhasama nao hadi kuwachukulia kama wanyama” Alisema Ncikazi.
“Siwezi kuomba msamaha kwa matukio ambayo kweli yanatokea Afrika, Niliomba msamaha kwa kuwasema nilivyowasema eneo lisilo sahihi” Alimaliza Ncikazi
Kocha huyo alilalamikiwa na Klabu ya Simba kwa kutoa kauli zenye nia ya kuichafua Simba mara baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali ambapo Orlando Pirates ilipoteza kwa bao 1-0 bao lililofungwa kwa mkwaju wa penati na Shomari Kapombe baada ya Bernard Morisson kuangushwa kwenye eneo la hatari.
